Friday, December 21, 2012

RUHUSU MAPENZI YA MUNGU YATIMIE KUHUSU MWENZI WA MAISHA YAKO.



Najua yumkini upo njia panda kwa habari ya kuoa au kuolewa. Si kwa sababu hakuna mtu wa kuoa au kukuoa, bali ni kwa sababu kila anayekuja ni tofauti kabisa na kile ambacho wewe unapenda na unafikiri pia ni mapenzi ya Mungu iwe utakavyo. Huenda kibinadamu kuna sifa/vigezo ambavyo ulijiwekea vya mtu ambaye ungependa kumuoa au kuolewa naye, lakini kila unapoomba unaona mtu anayekuja ni tofauti kabisa na vile ulivyotaka wewe. Na unapoomba zaidi kumhoji Mungu anakuhakikishia kwamba huyohuyo ndiye mtu wa mapenzi yake.
Hukuishia hapo umeshirikisha na wapendwa wenzako au hata watumishi wengine wameomba nao wamethibitisha huyo ndiye mtu wa mapenzi ya Mungu kwako. Kila unapojitahidi kufikiri kumwacha unakosa amani. Mimi ninakushauri inapofika mahali kama hapo we ruhusu tu mapenzi ya Mungu yatimie kwako. Zipo sababu nne za msingi  zinazonifanya nikushauri hivyo;
  • Mapenzi ya Mungu ndio utimilifu wa kusudi lake kukuleta wewe duniani.
Haukuja duniani kwa sababu ni kawaida ya wanadamu kuzaa, bali ni kwa sababu ni Mungu alikusudia wewe uzaliwe.Hii ina maana lipo kusudi la Mungu kukuleta duniani. Na ili kusudi lake liweze kufikiwa ni lazima ujifunze kuishi maisha ya mapenzi yake. Uishi ili kutimiza mapenzi yake hapa duniani.
Ni mapenzi ya Mungu pia kuhakikisha unaoa/kuolewa na mtu ambaye anajua mtasaidiana katika kutekeleza makusudi yake hapa duniani. Kwa hiyo si suala la kuoa au kuolewa unavyotaka, bali ni kuoa au kuolewa kwa mapenzi yake.
  • Mapenzi ya Mungu si lazima yakubaliane/yaendane na ya kwako.
Ni muhimu ujue kwamba mapenzi ya Mungu si lazima yaendane na ya kwako. Na hii ni kwa sababu mawazo yako si mawazo yake na njia zake si njia zako (Isaya 55:8). Jua kabisa mapenzi ya Mungu si lazima yakupendeze, yakufurahishe au yalinde heshima yako.
  • Kuna nyakati ambazo mapenzi ya Mungu kuyapokea ni machungu, yanaliza, yanafadhaisha, yanaogopesha.
Katika kuyakubali au kuruhusu mapenzi ya Mungu yatimie wakati mwingine     yanaweza kuwa machungu, kukufadhaisha, kukuliza, kukuumiza, kukuogopesha au hata kukuabisha kwa jinsi ya kibinadamu.
  • Mapenzi ya Mungu yanalenga kuleta heshima na utukufu kwake.
Ingawaje yanaumiza, kufadhaisha au hata kuaibisha kwa jinsi ya kibidamu /kiheshima/kimahusiano/kijamii /kiuchumi nk. Na hata kama  kwako yana athari kiasi gani uwe na uhakika mapenzi ya Mungu yanalenga kuleta heshima na utukufu kwake, hii ina maana HAYO NDIYO MAPENZI YAKE na si ya KWAKO. Tunapoomba kusema mapenzi yako (Mungu) yatimizwe ina maana mapenzi/matakwa ya kwetu (wanadamu) yasitimie.
Hebu tuangalie mifano kadhaa ndani ya Biblia;
Mfano wa Yakobo - Mwanzo 29:15-31.
Hii ni habari ya Yakobo alipokwenda Harani kwa Labani nduguye. Labani alikuwa na binti wawili, mkubwa aliitwa Lea na mdogo aliitwa Raheli amabye alikuwa na uso na umbilie zuri. Raheli ndiye ambaye Yakobo alimpenda na alikubali kutumika kwa miaka saba ili apate kumuoa. Baada ya miaka saba, Yakobo alipewa Lea ambaye hakumpenda kama mke bali alimpenda Raheli. Ingawa zilipopita siku saba ndipo alipopewa na Raheli kama mke wa pili.
Nikuulize swali, je Yakobo angeambiwa atumike miaka saba kwa ajili ya kumpata Lea, angekubali? Je unafikiri ni kwa nini Mungu aliruhusu Yakobo  mtumishi wake kufanyiwa hili? Sababu kubwa ni hii, ilikuwa ni mpango/mapenzi ya Mungu Yakobo amuoe na Lea pia. Hii ni kwa sababu ya umuhimu wa watoto aliowazaa ukihusianisha na uzao/ukoo wa Bwana wetu Yesu Kristo. Namaanisha kupitia Lea, Yakobo alizaa naye watoto wane, mmoja wao aliitwa  Yuda. Ukifuatilia ukoo wa Yesu Kristo utalikuta jina la Yuda linajitokeza (Mathayo 1:2). Kwa hiyo japo Yakobo hakumpenda Lea kabisa lakini Mungu alitaka na akajua kupitia wao atazaliwa Yuda ambaye ni kiungo muhimu katika uzao wa Yesu Kristo.
Mfano wa nabii Hosea – Hosea 1:1-4
Mstari wa pili unasema ‘… Bwana alimwambia Hosea enenda ukatwae mke wa uzinzi…’ Ukisoma hii habari yote utaona jinsi Mungu alivyomwagiza Hosea kwenda kuoa mawanamke mzinzi na aliyekubuhu kwenye dhambi hii. Sasa kwa jinsi ya kibinadamu haikuwa rahisi kulikubali. Lakini kwa sababu ilikuwa ni jambo la MAPENZI YA MUNGU ili mlazimu akubaliane nalo hata kama yeye hakutaka. Na ukiendelea kusoma sura za mbele utaona fundisho na uponyaji ambao ulitokea kwa watu wa taifa la nabii Hosea kutokana na utiifu wake katika mapenzi ya Mungu.
 Mfano wa nabii Samweli – 1Samwel 16:1-13.
Hii ni habari inayoelezea agizo la Mungu kwa Samweli kwenda kwenye nyumba ya Yese kumtia mmoja wa watoto wake mafuta kuwa mfalme wa Israel baada ya Mfalme Sauli kuasi. Yese alikuwa na jumla ya wana nane wa kiume, Mkubwa  wao aliitwa Eliabu na mdogo aliitwa Daudi. Sasa Samweli alipofika kwa Yese, Yese aliwaita watoto wake wote isipokuwa Daudi aliyekuwa anachunga kondoo wa babaye, akaanza kuwapitisha kwa Samweli ili amtie mafuta yule ambaye ndio mfalme.
Alipopita mtoto wa kwanza, nabii Samweli akasema moyoni mwake Yakini masihi wa Bwana yupo hapa mbele yake, kwa lugha nyepesi alisema yamkini huyu ndiye Mfalme ninayepaswa kumtia mafuta. Je Mungu alimjibu nini alipowaza hivyo moyoni mwake. Mungu alimwambia ‘usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. Bwana haangalii kama mwanadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo’. Mwishowe walipita watoto wote saba na Bwana akawakataa, hadi alipofika Daudi aliyetiwa mafuta.
Jifunze yafuatayo kutoka kwenye mifano hii mitatu;
  • Upo duniani sasa kwa ridhaa/ruhusa/mapenzi ya Mungu.
  • Na kama upo kwa ridhaa yake, ni lazima uishi kwa uongozi wake (Zab 32:8).
  • Thamani ya maisha yako ipo katika kuyatenda mapenzi ya Mungu.
  • Ni kipaumbele (priority) cha Mungu kujua nani atakuwa ni mkeo au mumeo. Sio suala la kuoa au kuolewa unayotaka wewe.
  • Mtazamo wako kuhusu mkeo au mumeo sio mtazamo wa Mungu. Ndoa yoyote anayo iunganisha Mungu ameshaiangalia mpaka mwisho wake.
  • Hivyo anapokupa mtu wa aina fulani, hata kama haendani na vigezo vyako, kumbuka lengo lake sio kukukomoa au kukuhuzunisha bali ni kuhakikisha anachotaka/mapenzi yake na si ya kwako yanatimia.
  • Smweli na Yakobo walitaka kukosea kwa sababu ya maumbile na mvuto wa sura kwa nje. Angalia sababu kama hizi zisikufanye ukaharibu mahusiano yako na Mungu na hivyo kukwamisha makusudi yake duniani.
  • Japo lilikuwa ni jambo gumu kwa Hosea kulikubali kibinadamu, yeye alitii na akabarikiwa kwa kulitumikia shauri la Bwana katika kizazi chake.
  • Ni mfano wa mfinyanzi na vyombo alivyovifanya. Mfinyazi ndiye anayejua sababu na matumizi ya chombo alichokifanya. Kazi yake huyu mfinyazi ni kuhakikisha lengo la ubunifu/uumbaji wake linafikiwa.
  • Na Mungu ndivyo alivyo, yeye ndiye aliyekufanya na anajua unachotakiwa kufanya hapa dunani, kazi yake ni kuhakikisha anakuongoza na kukuweka kwenye mazingira ya kusudi lake kupitia wewe kufanikiwa. Sasa mazingira au uongozi huo ni pamoja na kuhakikisha unaoa au kuolewa na mtu wa mapenzi yake.
  • Mtu wa mapenzi yake anaweza akawa tofauti na ulivyokuwa unataka. Ndugu yangu inapofika uko mahali kama hapa “the only option/alternative ni kuruhusu mapenzi yake yatimie na si kulazimisha yako kutimia”. This means there is no an option or alternative, you cannot escape it (Je unakumbuka habari za Yona, au Yesu pale Gethesemane?). Let his will be made in your life i.e.   Totally submit yourself to his will.
  • Usipokubali wakati una hakika hayo ni mapenzi ya Mungu kwako maana yake umeasi, ukiasi unatafuta matakwa yako na si yake. Mungu hata kulazimisha kuyatii mapenzi yake ila atakushauri kwa njia mbalimbali na mojawapo na mafundisho kama haya. Ukikataa ushauri wake ujue huko unakoenda yeye/uwepo wake hauko pamoja na wewe. Je unajua gharama ya kukosea au kutokutii mapenzi ya Mungu katika hili? Waulize wanandoa waliokosea ndio utajua madhara yake.
  • Naamini ujumbe huu umekuongezea maarifa na ufahamu wa kukusaidia katika kufanya maamuzi. Zaidi ni imani yangu kwamba kama ukijua hakika haya ni mapenzi ya Mungu kuhusu mwenzi wako basi utahakikisha yanatimia. Haijalishi hayuko unavyotaka, ndugu zako, ukoo wako, kanisa au hata Mchungaji wako hawamtaki, kama unahakika ni mtu wa mapenzi ya Mungu mpendwa nakushauri RUHUSU MAPENZI YA MUNGU YATIMIE, KINYUME CHA HAPO NI MAJUTO.
  • “Asomaye na afahamu, msukumo ambao nimeupata kuhusu kuandika ujumbe huu haukuwa mdogo, ni kama nilikuwa naambiwa hakikisha ujumbe huu unakamilika haraka iwezekanavyo ili kuwapa maarifa haya watu wangu”.
 Mwenye sikio na asikie lile ambalo Roho wa Yesu anasema na kanisa. Amen.

No comments:

Post a Comment